Cart (0)

Moshi Angani: Sehemu ya I 

Walikutana sokoni, mahali pa kelele na harufu ya matunda yaliyooza, lakini mioyo yao ilinyamaza kwa mshangao. John alikuwa mchuuzi wa karanga, na Agness alikuwa mrembo aliyekuwa akipita tu kununua vitunguu. Macho yao yalikutana tu mara moja, lakini yalizungumza mengi kuliko maneno.

 

Kila siku Agness alirudi sokoni, si kwa sababu ya vitunguu, bali kwa sababu ya tabasamu la John. John alianza kung’ara zaidi kila alipoona kile kivuli cha Agness kikipita mbele ya meza yake.

 

Wakaanza kuzungumza maneno mafupi, kicheko kidogo, na hatimaye namba za simu. Usiku ulichukua nafasi ya mchana, na ujumbe wa mapenzi ukawa jua la mioyo yao. Walipendana kwa haraka, kwa nguvu, kana kwamba dunia ingeisha kesho.

 

Lakini mapenzi mengine huwa kama moshi hufunika anga, hufanya kila kitu kiwe na harufu ya matumaini, lakini mwishowe hutoweka kimya kimya. John alianza kubadilika. Simu hazikupokewa. Agness alianza kujiuliza maswali yasiyo na majibu.

Mpaka siku moja, alipomkuta John akiwa na msichana mwingine, wakicheka kama vile walivyowahi kucheka pamoja. Alimwangalia tu, macho yakiwa na ukungu wa huzuni.

 

Kwa nini? aliuliza Agness

 

John hakusema chochote. Aligeuka, akakumbatia msichana wake mpya, na kuondoka kama moshi unaopeperuka angani hautarudi tena, hauwezi kushikwa.

Agness alibaki pale, moyo wake ukiwa umeyeyuka, lakini machozi yake yalionyesha maumivu moyoni mwake. Baadae alikumbuka kwamba hata moshi huacha harufu kabla haujatoweka.