Cart (0)

Moshi Angani: Sehemu ya III

 Moyo Usiopotea 

Mwaka mmoja ulikuwa umepita tangu mazungumzo ya mwisho kati ya Agness na John. Maisha yalikuwa yamebadilika. Agness sasa alikuwa mshauri wa vijana waliovunjika moyo, akitumia hadithi yake kama darasa. Aliandika kitabu kidogo kilichoitwa Moshi Angani: Hadithi ya Moyo Uliojifunza Kupumua Tena. Kitabu hicho kilianza kusambaa katika shule na vikundi vya vijana.

 

Siku moja alipata mwaliko kuzungumza kwenye taasisi moja ya vijana waliokuwa wanapitia changamoto za maisha, mapenzi, na mwelekeo wa maisha. Alipofika, aliambiwa kuwa kuna mgeni maalum ambaye pia alikuwa mzungumzaji wa siku hiyo na jina lake lilimshtua kidogo: John Musa. 

Alijaribu kujituliza. Nafsi yake ilikuwa tayari imepona, lakini hakuweza kujizuia moyo kupiga kwa kasi alipomwona John akipanda jukwaani. Alikuwa amekomaa, macho yake yalikuwa ya utulivu na yaliyosheheni hekima tofauti kabisa na John wa zamani aliyewahi kupoteza mwelekeo.

 

John alisimama mbele ya vijana na kusema:
Kuna wakati nilidhani kupenda ni kujifurahisha tu. Lakini sasa najua kupenda ni kujitoa, kuheshimu, na kulinda moyo wa mwingine kama wako. Nilijifunza somo hilo kwa njia ngumu. Na leo, nipo hapa si kwa sababu ya ushindi, bali kwa sababu ya majuto yaliyonifanya kuwa bora.

 

Baada ya hotuba hiyo, Agness alipanda jukwaani, na bila kumtaja jina John, alizungumza kuhusu thamani ya kujipenda, kujiheshimu, na kujiponya baada ya kuvunjika moyo. Wote walizungumza kwa sauti tofauti, lakini ujumbe wao uliungana mapenzi ya kweli huanza ndani ya mtu mwenyewe.

 

Baada ya hafla, walikutana tena, kwa mara ya kwanza bila maumivu, bila maulizo. Walikumbatiana kimya, kisha John akasema:
Leo nimefurahi kukuona ukiwa mzima, ukiangaa zaidi ya siku zote.

Agness alitabasamu:
Na leo nimejua, moshi wa zamani huweza kubadilika kuwa mwanga wa leo tukijifunza kutokana nao.

Walitengana wakiwa na amani. Hawakurudiana, lakini walielewana. Kwa sababu hadithi yao haikuhusu mapenzi tu bali kukua, kupona, na kuelewa kuwa si kila aliyepita maishani mwako alikuja kukaa, lakini kila mmoja alikuja kwa sababu.