Cart (0)

Moshi Angani: Sehemu ya I I

Agness alibaki pale sokoni, moyo wake ukiwa umeyeyuka, machozi yakilowesha mashavu yake kama mvua ya ghafla. Alijua mapenzi yao yameisha, lakini hakuelewa kwa nini yameisha kwa ghafla kama moshi uliofukiwa na upepo.

 

Miezi ikapita. Agness alijifunza kuishi bila ujumbe wa  usiku mwema  kutoka kwa John. Alijifunza kutabasamu tena, si kwa sababu ya mtu mwingine, bali kwa sababu alijifunza kujipenda mwenyewe zaidi. Alianza kuandika mashairi, akaungana na kikundi cha vijana waliopitia maumivu ya mapenzi, na polepole, aligeuza maumivu kuwa msukumo wa ndani.

 

Siku moja, akiwa kwenye kongamano la vijana, alishangaa kumuona John. Alikuwa amebadilika macho yake hayakuwa na nuru ile ya zamani, uso wake ulikuwa na huzuni iliyojificha nyuma ya tabasamu bandia.

 

Baada ya hotuba, John alimfuata Agness na kusema:
 Samahani… nilikosea. Nilikuwa kijana niliyeogopa kujitoa kweli. Lakini sasa najua, nilipokupoteza, nilipoteza zaidi ya mpenzi. Nilipoteza rafiki, na mwenza wa kweli.

 

Agness alimtazama kwa utulivu, kisha akasema kwa sauti ya upole:
 John, mapenzi yetu yalikuwa kama moshi yalifunika kila kitu kwa uzuri wa muda mfupi tu, lakini hayakuwa thabiti kushinda upepo wa maamuzi mabaya. Haukuumia wewe bali uliumiza sisi. 

Akatabasamu kidogo, akamgeukia na kuongeza:
 Lakini nashukuru. Kwa sababu kupitia maumivu hayo, nilijifunza thamani ya moyo wangu. Na sasa, sihitaji mtu kunipenda ili nijue thamani yangu. Nimejifunza kujipenda mwenyewe 

 

John alibaki ameduwaa, macho yake yakimtazama Agness akiondoka,  si kwa hasira, bali kwa nguvu mpya. Alitambua kuwa moshi wao uliwahi kuwa wa kipekee, lakini sasa Agness alikuwa taa inayowaka yenyewe, bila kutegemea moto wa mtu mwingine.